Baada ya Streams Milioni 2.4, Stans Sio Jina Jipya Tena

Stans kwa mara ya kwanza alifika kwenye masikio ya wasikilizaji wa Bongo Fleva kupitia wimbo “2025” wa Marioo, uliopo kwenye albamu The Godson. Wimbo huo, uliomshirikisha Stans, umefanikiwa kuvuka zaidi ya streams milioni 2.4 ndani ya kipindi cha mwaka mmoja, hatua iliyomweka Stans moja kwa moja kwenye rada ya mashabiki na wadau wa muziki.

Baada ya kimya kilichoibua maswali mengi, Stans sasa anarudi rasmi na kazi yake binafsi, “SAWA”, wimbo unaoifanya discography yake kufikia nyimbo mbili pekee kwa sasa. Ingawa idadi hiyo ni ndogo, matokeo yake sio kitu cha kuchukulia poa. kabisa.

Kwa mujibu wa takwimu za Spotify, Stans anafikia wastani wa wasikilizaji zaidi ya 43,000 kwa mwezi, idadi ambayo mara nyingi huonekana kwa wasanii wenye uzoefu wa muda mrefu kwenye game. Kwa msanii mpya, hii si bahati mbaya, bali ni matokeo ya mchango wake mkubwa kwenye wimbo 2025, ambao umeendelea kuwa lango lake kuu kuelekea soko pana la muziki.

Kuwa na discography ndogo lakini yenye wimbo uliovuka streams milioni 2.4 ni ishara chanya kwenye muziki wa kidigitali. Ni taa ya kijani kwa msanii chipukizi, ikionyesha wazi kuwa nafasi ya Stans kuendelea kung’aa kwenye majukwaa makubwa ipo wazi na ina msingi uliojengeka imara.

Chini ya Bad Nation Record Label, Stans anajitambulisha kama sehemu ya kizazi kipya cha wasanii wanaochanganya sauti, uhalisia wa hisia na mwelekeo wa kimataifa. SAWA sio tu wimbo mpya, bali ni hatua ya kwanza ya safari yake rasmi kama msanii anayejitambua, mwenye mwelekeo na malengo makubwa.

Kwa msingi aliouweka kupitia 2025 na sasa SAWA, macho ya tasnia yanaangalia hatua yake inayofuata, kwani dalili zote zinaonyesha kuwa Stans hajafika tu, bali amekuja kufanya vitu.

Post a Comment

Previous Post Next Post